Wednesday, September 22, 2010

NAFASI YA MTOTO KATIKA JAMII ISIYOMJALI

Inawezekana kabisa kuwa jamii imechoka hata kusikia habari za watoto, huenda watu wakawa hawako tayari hata kutaka kujua mambo mbalimbali yanayotokea kwa watoto na huenda jamii haina hata mikakati maradufu ya kuhakikisha utetezi wa haki za mtoto ni jambo la muhimu katika majira na nyakati zetu. Nadhani hata katika hatua na ngazi ya kwanza kabisa ya familia, mambo ya mtoto na nafasi yake katika familia si vitu vya kuzingatiwa sana. Hii ni picha ndogo na picha kubwa yake ni ukweli kwamba kama mtoto hajapewa nafasi katika familia atawezaje kupewa nafasi katika jamii kubwa inayomzunguka.
Mtoto anaweza kuwa wa kike au wa kiume, mrefu au mfupi, wa rangi yoyote, kabila lolote, dhehebu au dini yoyote, tajiri au masikini ili mradi tu awe na umri chini ya miaka kumi na nane (kwa tafsiri ya andiko hili). Pengine kwa tafsiri za mashirika mengine mtoto ni chini ya miaka kumi na nne (14) au kwa namna yoyote ile ambayo wewe binafsi na au pamoja na jamii yako mnamtafsiri mtoto kwa namna hiyo. Cha muhimu hapa ni kumzungumzia mtoto kama unavyoelewa na la muhimu zaidi katika makala hii ni Nafasi ya huyo mtoto katika jamii isiyomjali labda tu kama unaona jamii inamjali tena kiasi cha kutosha. Lakini huenda ukaona kama jamii yetu inamjali, sikatai labda tu ni kwa kiasi gain na ukaribu gani wa kumjali na pia hebu tutake kujua neno jamii linamaana gani ndipo tupate kujua kama ni kweli au la kwamba jamii haimjali mtoto.

Ni muhimu kumjua na kumtambua mtoto kwa namna unavyoweza ili kupunguza madhara ambayo watoto wanayapata kwa kutokuwa na ufahamu tu. Kukosa ufahamu ni kubaya na kunaumiza sana maana kinyume chake ni kuwa na ujinga wa kumtosha mtu kiasi cha kutotaka hata kushauriwa. Na alama ya muhimu na huenda ya kwanza kabisa ya mjinga au mpumbavu ni ujasiri wake wa kutotaka kushauriwa, ujasiri wake wa kujiona kuwa hawezi kukosea jambo na huu ni umasikini wa hali ya juu sana. Kuna mambo mengi sana ya kujiuliza juu ya nafasi ya mtoto katika jamii isiyomjali. Kwanza watoto wamekosa watu madhubuti wa kuwatetea na kuwasemea kwa moyo mmoja bila kuingiza matakwa yao binafsi. Hawa watu wapo wachache sana kiasi kwamba wengi zaidi yao wanahitajika na ndio maana mtu kama huyo akifanya jambo lolote ni rahisi tu kujulikana maana ni wachache.
Pili, watu wamekuwa na moyo wa kutojali maana wengi wamejikatia tama ya kuishi au ya kuiona Tanzania mpya. Mimi sio tu kwamba naamini kuwa Tanzania mpya iko njiani inakuja bali pia nina hakika kuwa hilo liko hivyo na si vinginevyo. Tunamiaka michache tu ya kuiona Tanzania iliyojaa taarifa mbalimbali za uovu na ufisadi katika maeneo yote na hata kusikia watoto wadogo kabisa wa miaka chini ya mitano wakibakwa. Muda umekwisha, usiku umeendelea sana na sasa tazama ni mchana mweupe pee. Kama unasoma haya maandishi na umekata tama nakushauri kwa upendo kuwa uwazavyo sio na muombe Mungu akusaidie uishi miaka ishirini ijayo ili uwe shuhuda pamoja na wengi wanaotazamia kuzaliwa kwa taifa la Tanzania. Na njia pekee ya kulizaa taifa jipya la Tanzania ni kuwekeza kusiko na unafiki kwa watoto na vijana wetu.
Tatu mtoto anaunganishwa na taifa moja kwa moja. Sio tu yeye ni taifa la kesho kinadharia bali yeye ndiye kesho yenyewe, yeye ndo msingi, yeye ndo urithi wenyewe, mtoto ndio uthibitisho wa kuwepo kesho yaani kizazi kijacho kinategemea watoto. Unaweza kuwaza kama Mungu akizuia watu kuzaa na kupata watoto itakuwaje? Lugha yake ni rahisi tu, hiyo itamaanisha kuwa Mungu anataka awamalize kabisa wanadamu maana hakuna kizazi kinachoendelea. Usishangae kwanini namtaja sana Mungu maana wengine walio vipofu anaweza tu akakwazika na kuumia kwa sababu namtajataja sana Mungu, sasa unataka nimtaje shetani? Namtaja Mungu kwasasbabu moja kubwa: ndiye ninaye mwamnini na kumtegemea na sio mwingine kwa hiyo sahau kwamba kwa namna yoyote ile nitamtaja shetani au yeyote afananae. Kwa sababu hiyo Mungu anataka tuendelea kuishi na ndo maana ameruhusu vizazi viendelee kuwepo na kuja na hiyo inaonyesha nafasi ya mtoto katika moyo wa Mungu.
Jamii ni mazingira yanoyomzunguka mtoto, ni watu wanaoishi au kuwepo mahali ambapo yeye mtoto yupo kwa wakati huo wa kudumu au wa muda mfupi, kwa mfano jamii ya kwanza kabisa ambayo mtoto anakutana nayo hata kabla hajazaliwa ni mama yake, pale anapokuwa tumboni mwa mama yake. Akizaliwa anakutana na jamii kubwa zaidi ya familia yake na hii ndio hasa hutengeneza mazingira ya makuzi na malezi ya mtoto kwa mara ya kwanza kabla mtoto hajajihusisha na jamii kubwa zaidi. Pia akitoka kwenye familia mtoto anakutana na jamii kubwa zaidi ya marafiki anapokuwa maeneo mbali mbali kama shule, kanisani, michezoni, anapotembea, akiwa kwenye usafiri na hata akiwa kwenye mikusanyiko mbalimbali. Na kwa kadri ya namna mtoto anavyokua ndivyo jamii yake inavyopanuka zaidi na kumfananisha nayo. Hapa tunaweza sasa kusema kabisa kimpangilio mgawanyo wa jamii anayokulia mtoto toka ya kwanza mpaka ya mwisho na hii itatusaidia sana kubaini ni wapi tatizo linaanzia na nini basi kifanyike sasa.
Mgawanyo wa jamii anamokulia mtoto

Kama nilivyoelezea hapo juu utaona na hata ukitaka kuthibitisha hili ninalosema wewe mwenyewe ulishawahi kuwa mtoto na ulipokuwa unakua kuna jamii fulani ulikutanishwa nazo na au ulikutana nazo. Kwahiyo hapa chini nitazipanga jamii hizo kwa mpangilio na pia kutokana na umuhimu wake kwa makuzi na malezi bora ya mtoto.

1. Tumboni mwa Mama

Nafasi ya mtoto kaatika jamii isiyomjali ni swala refu sana na huanzia mahali ambapo watu wengi hawatilii maanani sana, tumboni mwa mama. Hapa mtoto anakuwa katika hali ya mimba na ni rahisi tu kuona kuwa mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake hayuko katika jamii lakini mimi nakwambia tayari anakuwa ni sehemu ya jamii kwani ni kiumbe hai na jamii inakuwa inamsubiria kufika kwake na tena inampigia na mahesabu yake. Kwa maana hii thamani na utu wa mtoto unaanzia tumboni mwa mama, akiwa hata hajazaliwa na hapa duniani kuna watu huwangojea watoto wao kwa hamu kubwa sana na wengine huamua hata kuwaua kwa kutoa mamba.
Mtu yeyote anaehusika katika mchakato wa kutoa mimba (Kiwango cha juu cha uuaji) sio kwamba tu anajisaliti yeye mwenyewe bali anamsaliti Mungu aliyempa uwezo wa kupata mimba, anmsaliti mtoto wake mwenyewe na watoto wengine walio katika hali hiyo ya mimba, anaisaliti jamii inayotarajia kuja kwa rais au waziri mkuu huyo, anafanya usaliti katika mabo yote na hali zote za binadamu. Inahitaji ujasiri wa kishetani kufikia hatua hiyo ya uuaji maana kazi za shetani ni tatu tu, kuua, kuchinja na kuharibu na nisikitiko kuona kwamba mawakala wa shatani wamekuwa wengi kiasi cha kutisha. Maana mawakal hawa wako kila mahali, manyumbani, kanisani, misikitini,mashuleni, makazini,mitaani,serikalini,wako pia Tanzania (na katika mikoa yake yote) na dunia nzima, ni Furaha iliyoje kwa shetani!.
Watu wanaotoa mimba, watu wanaosaidia wengine kutoa mamba, watu wanaoona kuwa kutoa mimba ni suluhisho la matakwa yao kwa wakati huo na mtu yeyote anapigania haki za utoaji mimba sio kwamba tu amekosa ufahamu juu ya mtoto na haki zake bali ni mzigo kwa akili zake mwenye, ni mjinga kwa ufahamu wake mwenyewe na muuaji kwa upumbavu wake mwenyewe. Mtu wa namna hii ni hatari kuishi nae kwani kuua yeye sio swala kubwa sana, unaweza ukalala nae na usiku akaamka akachukua kisu akakuua. Napenda niseme hapa kuwa hakuna sababu yoyote inayofaa au kupendeza ambayo kwayo twaweza kusema ni salama kuua kwa mfumo wa utoaji mamba.

Huu ni upungufu wa maadili, hekima, ufahamu na utu na ndio maana mtoto hana nafasi yoyote kwa maana jamii haimjali. Kama jamii inamjali mtoto haiwezi kuruhusu uuaji katika mfumo wa kutoa mamba maana hata akiwa tumboni anaitwa mtoto na wakifanya vipimo hospitali anaonekana akipumua, akila na tena akiwa wa kike au kiume. Uuaji ni dhambi na kuwa na dhambi ni kuwa na uadui na Mungu na mwisho wake ni jehanamu ya moto na mateso ya milele na hapo haijalishi ni mtoaji mamba, ni aliyemshauri, ni aliyempa pesa kwenda kutoa, ni mvulana aliyekataa kuwa mimba si yake hivyo binti akawa na hasira mpaka akaenda utoa mamba au mtu yeyote yule wa ngazi yeyote ile katika jamii. Sina shaka kwamba wote wanofanya hivyo watalipwa kwa kadri ya wanavyopanda. Namaanisha kuwa hakuna sababu ya kuvutia inayoweza kufanya utoaji mimba uonekane ni jambo jema na kutufaa sana katika jamii yetu, kumbuka kuwa kuwa huru kunaenda na kuwa na nidhamu katika uhuru uliopewa (Freedom is about Discipline and not misbehaviors) kwahiyo usije ukautumia uhuru wako kwa kufanya yasiyo pasa.

Katika hali kama hizi ni nini nafasi ya mtoto katika jamii kama hii isiyomjali, jamii isiyotaka hata kumuona kwa macho na iko tayari kumuua akiwa tumbani mwa mama? Ni ajabu kuona katika jamii hii kwamba watu wameenda kusomea namna nzuri za utoaji mimba, namna nzuri za kuwashauri watu kutoa mimba badala ya kuwashauri namna nzuri za kutopata mimba na kama uwezo wa kupata au kutopata mimba uko mikononi mwao. Mtoto hana nafasi katika jamii hii lakini bado watu wengi na mashirika yasio na yaliyo ya kiserikali yanatengeneza pesa nyingi kwa matumizi yao binafsi kwa kupitia mgongo wa mtoto. Hakika mtalipwa na mimi nitakuwa mmoja wa watakaoshuhudia mnavyolipwa hapahapa duniani. Huu ni ujumbe wenu na tena ni bora usingesoma waraka huu, kwakusoma kwako ndio umetangaza kuwa ni mwisho wa wewe kufanya hayo uliokuwa unafanya. Ukiamua kuendela kuyafanya wewe fanya tu lakini nakuhakikishia kuwa jicho la Bwana Mungu linakutizama na litakufuatilia mpaka utakaporudi kwake au umkatae milele.
Tunawezaje kuwa na ujaisri wa kusema tunawapenda watoto wakati tunakula pesa zao? Tunanunua magari ya kifahali na majumba makubwa kutoka kwenye pesa za watoto, hii ni ajabu sana. Mbona vifo vya watoto vinaongezeka kila siku? Wengi wao wanakufa na malaria, swali langu ni kuwa miradi yote ya kugawa vyandarua na pesa hizo zote zinaenda wapi? Mtanzania mwenzangu ni bora usingesoma waraka huu lakini kama umesoma na ujue tu kuwa ndo mwisho wako wa kufanya hayo uliyokuwa unafanya, amini usiamini. Utalipwa huku watanzania wote tunaona. Ni ajabu sana kuona nchi ya kwetu wenyewe, watoto wa kwetu wenyewe,sisi wenyewe ni wamoja na wazalendo wa nchi yetu leo hii wewe mtanzania unaiba fedha za watoto wa watanzania wenzako tena wale walio masikini kuliko wewe unaenda kujengea nyumba na kuwapeleka watoto wako kwenda kusoma nje, huu ujasiri unaupata wapi? Huu ujasiri hakuna mwanadamu aliyenao ni shatani tu.
Mama mjamzito anatunzwaje kama kweli tunajali kiumbe alichonacho tumboni? Ninyi akina baba mnaowapiga wake zenu wajawazito akili zenu ni zilezile mlizokuwa nazo wakati mnawachumbia? Je, mlipanga kupata watoto? Kama mlipanga mbona unampiga mkeo tena wakati ni mjamzito? Kwanini usingempiga kabla hajawa mjamzito? Hujui mtoto akiwa tumboni mwa mama yake hulia pamoja na mama yake? Ulishawahi kuliona chozi la mtoto akiwa tumboni mwa mama? Unajua atake lifuta hilo chozi? Hakika yako ni bora usingesoma waraka huu. Ni kweli jamii inamjali mtoto?
Wewe mama mjamzito unamlisha mtoto wako tumboni chakula gani? Sasa ndo nashangaa kwamba mama mjamzito anaenda na mtoto wake mpaka kilabuni na anamnywesha pombe, mataputapu huku akifurahia, hivi hujui unachokula wewe na mtoto wako tumboni anakula hicho hicho? Hujui kuwa utaalamu mwingi unapunguza mbao ya maana kuonekana hayana maana wala umuhimu wake? Kwanini unajuta kuipata hiyo mimba? Ni kweli kwamba kujuta kwako kumekufanya umuite mtoto wako Majuto? sasa huu ni utabiri wa kishetani kabisa,kwanini usimwite Baraka? Tafuta kujua watoto wote wenye majina kama Majuto,Shida,nk utaona maisha yao ya leo. Jifunze.

Ni kweli kwamba kila binadamu ana haki ya kuishi? Kwanini anaeua mtu kwa kisu au risasi anapelekwa gerezani na kuchukuliwa hatua kali za kisheria na mtu anaua kwa kutoa mimba anapongezwa kwa tafrija za ushindi wa sababu ya utoaji mimba? Tukia la uuaji likitokea mahali Fulani na vyombo vya dola vikienda sehemu ya tukio mtu yeyote atakae kutwa katika eneo hilo kisheria atashikiliwa na polisi akiisaidia polisi katika uchunguzi,sasa mbona mtu akitoa mimba si yeye wala aliyemtoa mimba,wala aliyempa mimba anashikiliwa kwa kitendo hich cha kinyama? Jamii inamjali kweli mtoto?
Dada zangu inakuwaje mimba upate mwenyewe kwa moyo mweupe, maana unajua kabisa unapofanya mapenzi ni vitu gani kadhaa vyaweza kutokea,halafu unaenda kuua bila hata woga wowote? Huu sio moyo wa mwanadamu. Wewe unazaa mtoto mchanga unamuweka kwenye mifuko tena mifuko ambayo hata serikali imeikataa ndo unaenda kumtupa jalalani,wewe ulitupwa? Kwani ukienda kuomba msaada kwamba jamani mimi sina uwezo wa kulea mtoto huyu nani mwenye utu atakaekataa? Ni nini nafasi ya mtoto katika jamii hii isiyomjali??

Nauliza hivi inakuwaje wewe mvulana unafanya ushirika wa kupata mtoto na binti halafu unaikataa hiyo mimba kwamba sio yako unakuwa unawaza nini? Unajua maana ya wewe kumkataa huyo mtoto? Unadhani utaikimbia hiyo mimba milele? Ulishasikia mtu ameikimbia damu yake? Unajidanganya.
2. Mama na Baba

Mtoto anapozaliwa tu anakukutana na mama yake kwanza. Wakati huu ni wakufurahi sana na kumshukuru Mungu kwa kumleta mwanadamu mwingine ambaye atakuwa mmoja kati ya watu mashuhuri sana nchini na duniani. Ni tukio zuri sana kwa majira haya na hivyo mama anakuwa jamii ya kwanza kabisa ya mtoto kuanza kusikia, kuona na kujifunza kwake. Kitu ambacho unaweza usikijue ni kuwa maneno yote unayoyasema mtoto anasikia. Anaefuata katika kupanua jamii hii ya mtoto ni baba. Mitizamo ya wazazi kwa mtoto anaekua ni ya maana nay a umuhimu wa pekee sana.
Maneno wazazi wanayokiri kwa habari ya mtoto wao ni muhimu maana ndiyo yanajenga msingi wa maisha ya mtoto wao. Ajabu zipo nyingi duniani na moja kati yazo ni kusikia mama au baba akimuita mtoto wake mbwa,Malaya,shoga,nyoka,mende,bwege na hata matusi makubwa ambayo hata mtoto mwenyewe anashangaa kwani ni lugha asiyoifahamu na hajizoea kwa namna hiyo. Matokea yake mtoto anakuwa katika maneno na matusi ya wazazi na hivyo tabia zake zinaendana na yote yaliyosemwa juu yake na wazazi wake.
Mpaka sasa nimeona vitu vya kwanza kabisa ambavyo watoto wengi huanza kusikia na kuona ni mambo yasiyo faa, matusi, picha za ngono, mambo ya ulevi, uzinzi na vitu vifananvyo na hivyo. Imenichukua muda sana mimi kuacha kutukana kwani toka nakua katika jamii ileile iliyokuwa hainijali nilianza kusikia mambo hasi zaidi ya chanya. Nilianza kumjua shetani na mambo yake kuliko Mungu na wema na upendo wake na ndio maana ni rahisi zaidi leo kusema habari mbaya kuliko nzuri. Kama huamini wewe leo nenda ukabake mtoto, uone jinsi dakika tano zinavyoweza kuitaarifu Tanzania na nchi za nje huo ubaya. Lakini ukiandika swala jema na la kuisaidia jamii kama hili utaona watu watakavyosaga meno ingawa kwa hili langu kusaga meno sio jibu, jibu ni mabadiliko ya mitazamo ya maisha na hali tabia.
Nawauliza wazazi,je ni sawa mtoto kuangalia vipindi vyoote katika luninga? Usalama wa mtoto wako uko wapi? Enyi wazazi mbona mnatuua sisi watoto wenu polepole kama vile sisi ni miti? Vipi kuhusu vipindi vya redio? Huu ni utandawazi? Mbona mnatulazimisha kushika imani zenu huku mkitupa uhuru wa mambo yasiyofaa? Sio mimi nashangaa peke yangu bali hata shetani mwenyewe anashangaa kuona baba na mama wanamchukua mtoto wao wanenda wote disco huku wakiielezea hiyo hali kuwa ndo maish ya kisasa. Ukweli ni kwamba sio vitu vyote vinavyofaa japo vyote ni vizuri na vinapendeza sana. Hata siku moja mzazi hajawahi kumsifia mtoto wake zaidi ya kumponda na kumdharirisha usiku kucha kama vile ni vyama vya upinzani. Inafika wakti sasa masikio na macho ya mtoto yanaota sugu na hapo sasa kibao hubadilika na mtoto anaanza kuonekana msumbufu kwa wazazi wakati uhalisia ni kwamba wazazi ndo waliomuandaa kuwa hivyo.
Wewe baba unajisikiaje kufanya ngono na mtoto wako mwenyewe? Ni raha kiasi kwamba huogopi kuwa unaweza kufa hapohapo katika tendo hilo na ukakutwa hapohapo? Hujui palipo na mizoga hapakosi kunguru? Umetumwa na Mganga? Kwanini huyo Mganga asikupe binti yake? Kwanini hutaki kufikiri? Huoni kama upumbavu wako mwenyewe unakumaliza na ujinga wako unakuangamiza? Hiyo ni laana, umelaaniwa wewe ufanyae hayo yote, umelaaniwa.

Utasema nimekutukana, wakati mimi nakusaidia utoke katika upofu wa macho yako na utazame uhalisia wa mambo na uache kufanya mabo kama mnyama. Ni ajabu unamtani mtoto wako? Unamnyemelea mtoto wako anapokuwa bafuni? Una akili kweli wewe? Unaangalia nae picha za ngono wakati mama yuko hospitali anaumwa, wakati mama kasafiri kwenda kumlipia ada ya shule? Baba ndio kichwa cha familia, je hii inamaana ufanye unavyojisikia? Utalipwa nasi tukishuhudia hapahapa duniani, huo moyo na ujasiri haupo kwa mwanadamu awae yote

Vipi mama unapomshauri mtoto wako kuwa mjanja mjini maana yeye anakitega uchumi? Huoni aibu kumuingiza mtoto wako kwenye biashara ya ukahaba? Au kwa sababu nchi nyingine wanafanya hivyo kwa hiyo hiyo inamaana hata wewe ufanye? Hujui kuwa kila mtu ataubeba mzigo wake mwenyewe? Mbona unataka kumtupa mtoto wako uliye kaa nae miezi tisa tumboni, hukumbuki ule uchungu wakati wa kujifungua? Yote hayo ulifanya bure,ili leo umuite mtoto wako Malaya,mbwa? Au unakipaji cha kutukana,kama ndio kaitukane miti basin a sio damu yako mwenyewe.
Laiti kama tungekuwa tunatembea usiku wa manane mitaani na kuona jinsi watoto wanavyopata shida kwasababu ya jamii isivyo mjali mtoto na hivyo kutompa nafasi inayostahili. Inafikia hatua hao watoto wanabatizwa majina,eti watoto wa mitaani,ni kweli ni watoto wa mitaani lakini hujui kuwa wametoka kwa baba na mama wa mitaaani pia? Unajua taabu ya kulala kwenye makorido ya nyumba za wahindi? Wewe sasa hivi unachakula na ndo maana huwezi elewa ninachokisema, nakushauri uwe makini maana haya mabo hubadilika kama upepo wa kiangazi.
Na hii eti ndo familia yake anayotakiwa kujifunza na kukua nayo, yaani kwa ujumla hi indo jamii yake ya karibu ambayo anatumia muda mwingi zaidi. Baadae wanakuja ndugu wengi na hasa kwa familia zetu za kiafrika. Udanganyifu huongezeka kadri watu wanavyozidi kuwa wengi nyumbani na hivyo ushawishi unaozidi kumfanya mtoto awe katika mazingira magumu zaidi
3. Imani na shule

Hapa mtoto huusishwa na namna fulani ya imani ya kimila au ya kisasa au dini au dhehebu fulani ili afanane na jamii hiyo. Na hapa ndio tunakutana na mambo kama ubatizo na kupewa majina yanayofanana na imani hiyo. Mtoto anapelekwa shule na mara nyingi chekechea na kuendelea. Wengine pia hupelekwa makanisani au kwenye mikusanyiko mingine ya kiimani ili kufundishwa mambo yanayouhusu imani.
Mashuleni mtoto anafundishwa elimu inayofanana na dunia hii ili aweze kuyakabili maisha na changamoto zake. Katika mambo ya imani mtoto anafundishwa mambo yasioonekana lakini ambayo ni ya msingi kuliko yanayoonekana. Anafundishwa juu ya imani ya wazazi wake hata kama inamfaa au haimfai. Utajuaje kuwa inamfaa au haimfai, wakati ambapo mtoto amekua na sasa anadhihirisha yale yote yaliondani yake na ambayo kwa hakika ndiyo aliyofundishwa. Sasa inakuwaje mzazi huyo huyo aliyemfundisha mtoto mambo hayo yote leo hii aje kusema eti watoto wa siku hizi wameharikbika kabisa?

Hapa nitaongea zaidi maana ni eneo la muhimu sana katika makuzi bora ya mtoto na ndo humjengea msingi wake wa namna atakavyokuja kuishi baadae.
4. Jamii ya ujumla

Hapa sasa ni pale mtoto anapokutana ma marafiki huko nje, anaazna kukutanana na njia mbali mbali za mawasiliano kama simu, mtandao na pia anapata taarifa nyingi zaidi. Mtoto katika jamii hii anakuwa anamaamuzi ya kuchagua vitu mbali mbali anavyovipenda, atachagua marafiki, atapata muda wa kuangali luninga katika vipindi mbalimbali vinavyoonyeshwa. Na pia anakuwa na uhuru wake wa ndani wa kufuata yale aliyoyaona na kuyasikia katika kukua kwake. Na huenda kuna mgawanyo mkubwa zaidi ya huu, huu nilioandika hapa ni mfano kwa ajili ya kuelezea kile ninachotaka kusema na ili tufike mahali tuone ni wapi panahitaji msaada ili kuhakikisha kuwa haki za mtoto zinalindwa na kutetewa.

No comments: